Jumanne , 19th Jun , 2018

Timu ya magari ya Red bull, imethibitisha kuachana na kampuni ya Renault ambayo ilikuwa inawatengenezea injini za gari zao mwisho wa mwaka huu na itaanza kufanya kazi na kampuni ya Honda ya nchini Japan.

Red Bull na Honda kwa pamoja wamesaini mkataba wa miaka miwili ambapo kuanzia mwaka ujao kwenye michuano ya mbio za magari duniani Formula One, Honda ndio watatengeneza injini za Red Bull.

Red Bull na Renault wamefanyakazi kwa pamoja kwa miaka 12 ambapo wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa dunia wa mbio za magari mara 4 mfululizo katika miaka ya 2010 na 2013.

Kampuni ya Honda sasa itafanya kazi na timu mbili kwa mara ya kwanza ambapo tayari inatengeneza injini za timu ya  Toro Rosso na sasa itaanza kutengeneza za Red Bull.

Honda wamepata mkataba wa kufanya kazi na Red Bull ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu timu ya McLaren wavunje mkataba na kampuni kwa madai kuwa injini zao zinawarudisha nyuma kwenye mbio za ubingwa.