Jumatatu , 21st Nov , 2016

Uongozi wa timu ya Tanzania Prisons umesema usajili ndani ya timu hiyo utafanyika mara baada ya kuipitia ripoti ya Kocha ili kuhakikisha unafanya marekebisho yatakayoleta faida ndani ya timu hiyo.

Tanzania Prisons

Afisa Habari wa Tanzania Prisons Oswald Morris amesema, mpaka sasa bado hawajaanza zoezi la kuangalia wachezaji ambao wanawahitaji kwani ripoti ya kocha itaelezea mapungufu ambayo yatasaidia kuweza kupata wachezaji ambao wataisaidia timu hiyo katika michuano ya ligi kuu ya Soka Tanzania bara.

Wakati huohuo Oswald amesema, hakuna kocha waliyefanya naye mazungumzo kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Kocha Abdul Mingange ambaye mkataba wake umemalizika na uongozi unatarajia kukaa na kufanya naye mazungumzo ili kujua kama ataendelea kukinoa kikosi hicho.

Oswald amesema, anaamini mzunguko wa lala salama wa ligi kuu ya soka Tanzania bara utakuwa ni mgumu kutokana na kila timu kuwa katika maandalizi kwa ajili ya mapambano ya kuweza kujiweka katika nafasi nzuri ndani ya ligi hiyo lakini kwa upande wao wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi kama ilivyokuwa kwa msimu uliopita.