Jumamosi , 17th Feb , 2018

Nyota wa Manchester United Paul Pogba ameondolewa kwenye kikosi cha timu hiyo kitakachoivaa Huddersfield kwenye mchezo wa FA raundi ya 16 baadae usiku wa leo.

Kocha Jose Mourinho amesema alimjumuisha Pogba kwenye kikosi lakini amelazimika kumwondoa kutokana na kuumwa ghafla japo hajaweka wazi ni ugonjwa gani umempata nyota huyo wa Ufaransa.

Baada ya kuondolewa kikosini nafasi ya Pogba  imechukuliwa na kinda Ethan Hamilton mwenye umri wa miaka 19 kutoka timu ya vijana ya Manchester United.

Katika mchezo huo wa leo Manchester United itakuwa ugenini kwenye uwanja wa  Kirklees, ambapo itakuwa inasaka nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Hata hivyo Mourinho hajasema kama ugonjwa aliopata Pogba unawezekana ukathiri nafasi yake kwenye mechi ya UEFA dhidi ya Sevilla kwenye uwanja wa Ramon Sanchez Pizjuan Jumatano ijayo.