Alhamisi , 15th Feb , 2018

Wachezaji wawili wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam 'ASFC' kutoka timu ya Singida United pamoja na Green Warriors wamefungiwa na kucheza mechi tatu na kutozwa faini ya laki tano kwa kila mmoja baada ya kubainika kutoingia uwanjani na timu zao

Hayo yamebainishwa na taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Mashindano hayo Efrem August kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), mchana wa leo alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya ofisi ya ofisi ya TFF na kusema baada ya Kamati ya mashindano ya TFF iliyokutana Februari 13, 2018 kupitia taarifa za mchezo kati ya Green Warriors na Singida United walibaini wachezaji Deus Kaseke wa Singida United na Shaban Dihile wa Green Warriors kuingia uwanjani bila ya kuwa na timu zao.

"Katika mchezo namba 73 uliyowakutanisha Singida United dhidi ya Green Warriors ilibainika wachezaji hao kutoingia uwanjani na timu zao pamoja na kutokuwepo wakati timu hizo zikipeana mikono kabla ya kuanza kwa mechi hiyo iliyofanyika mnamo Januari 31, 2018 katika uwanja wa Azam Complex Chamazi", amesema Efrem.

Aidha, Efrem amesema adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya ASFC (1) ambayo inaelekeza kutumika kanuni ya ligi husika na hivyo kanuni iliyotumika ni 37(7d).

Kwa upande mwingine, Efrem amesema mchezaji wa Singida United Kambale Salita amepelekwa kwenye kamati ya nidhamu ya TFF kwa kosa la kumpiga mchezaji wa timu pinzani kwenye mchezo huo.