Jumatano , 3rd Jan , 2018

Kiungo wa zamani wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania anayechezea klabu ya Mtibwa Sugar kwasasa Henry Joseph Shindika ameanza mazoezi rasmi leo baada ya kuwa nje kwa muda mrefu.

Katibu msaidizi wa Mtibwa Sugar, Abubakar Swabur amethibitisha kuwa Henry ameanza mazoezi baada ya kupona majeraha ya goti yaliyokuwa yanamsumbua kwa muda mrefu hali iliyompelekea kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Swabur amesema mchezaji huyo wa zamani wa Simba SC na Kongsvinger ya Norway, amepona kikamilifu hivyo kufanya idadi ya majeruhi katika kikosi cha Mtibwa kubaki watatu, ambao ni beki Salum Kanoni, kiungo Mohammed Issa ‘Banka’ na mshambuliaji Kelvin Sabato.

“Henry amepona vizuri kabisa na hata hawa majeruhi wengine watatu nao maendeleo yao ni mazuri, ni watu ambao tunawatarajia kurudi wakati wowote,” amesema.

Katibu huyo msaidizi pia ameongeza kuwa mlinzi wa kati wa klabu hiyo Stahimili Mbonde hayupo kwenye kikosi cha Mtibwa kwasasa akiwa na ruhusa maalum ya kushughulikia matatizo ya kifamilia.

Mtibwa Sugar inashika nafasi ya tano kwenye Ligi ikiwa na pointi 21 na inatarajiwa kushuka dimbani Januari 13 kumenyana na wenyeji, Lipuli kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa katika mchezo wa rauandi ya 13 ya VPL.