Jumanne , 8th Jun , 2021

Timu ya Brooklyn Nets imeibuka na ushindi wa alama 125 kwa 86 dhidi ya Milwaukee Bucks kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa nusu fainali ya ligi ya kikapu nchini Marekani kwa ukanda wa Mashariki kwenye mchezo uliochezwa usiku wa kuamkia leo.

Kevin Durrant wa Brooklyn Nets akirusha mpira nje ya eneo la D na kufanikiwa kuupita kwenye kikapu na kupata alama tatu '3-Point made' mbele ya Giannis Antetokounpo wa Milwaukee Bucks.

Nets imeibuka na ushindi huo mnono baada ya nyota wake tegemezi Kevin Durrant kuonesha kiwango bora na kuwa nyota wa mchezo kwa kufikisha alama 32 nyingi kwenye mchezo huo kuliko mchezaaji yeyote, rebaundi 4 na assisti 6 na kuibeba Nets kwa mara nyingine tena.

Bila hata ya uwepo wa mlinzi wake tegemezi James Harden anayesumbuliwa na maumivu ya misuli lakini Kyrie Irving hakuwa mnyonge kwani alififkisha alama 22, rebaundi 5 na assisti 6 na hata Blake Griffin aliyeanza mchezo huo alionesha kiwango bora na kushangaza wengi.

Griffin alikuwa mwiba mkali kwa Bucks licha ya kucheza dk25' pekee lakini alifanikiwa kupata alama 7, rebaundi 8 na assisti 1 ilhali upande wa Bucks, Giannis Antetokounpo alishindwa kuonesha cheche kali zaidi mbele ya Durrant kwani alipata alama 18, rebaundi 11 na assisti 4.

Katika kujikusanyia alama hizo, Durrant alirusha mpira mara 6 kujaribu kufunga nje ya eneo la D '3-Point made' na kufanikiwa kufunga mara 4 jambo lililomfanya aweke rekodi ya kushika nafasi ya saba kwa wachezaji wenye '3-Point made' nyingi zaidi 321 kwenye historia ya NBA ya muda wote.

Durrant anamfukuzia nyota mwenzake wa Nets, James Harden mwenye 336 na kushika nafasi ya tano, Lebron James wa Los Angeles Lakers mwenye 432 na kushika nafasi ya pili huku kinara wa mitupo hiyo ni Stephen Curry wa Golden State Warriors mwenye '3-point made' 470.

Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Brooklyn Nets ambao wanazidi kuendeleza moto wao kwenye michezo hiyo ya NBA Playoff na hata wengine kuwatabiria ubingwa, Bucks wanamlima wa kupindua matokeo kwani wanahitaji kuwasimamisha Nets kabla ya hawajaondoshwa.

Michezo ya mtoano ya NBA itakayoendelea leo kwenye mzunguko wa kwanza kwenye nusu fainali kwa ukanda wa Mashariki ni Philadelphia 76ers watakaokipiga na Atalanta Hawks saa nane na nusu usiku huku Utah Jazz watacheza na Los Angeles Clippers saa 11:00 Alfajiri ya kuamkia kesho.