Jumatatu , 18th Mar , 2019

Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na uwanja wa Wanda Metropolitano, jijini Madrid Hispania, vimeingia kwenye vitabu vya rekodi katika mashirikisho ya soka ya nchi husika na duniani baada ya kuingiza mashabiki zaidi ya 60,000 kwenye mechi zilizopigwa Machi 16, 2019.

Kwa upande wa uwanja wa Taifa ambao unaingiza mashabiki elfu 60 waliokaa, Machi 6, 2019, umeingia kwenye rekodi baada ya mashabiki wa Simba kuujaza uwanja huo kwenye mchezo wa mwisho Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita ambao ulimalizika kwa Simba kushinda mabao 2-1 na kufuzu robo fainali.

Kwa upande wa Wanda Metropolitano wenyewe umeingia kwenye vitabu vya rekodi za soka nchini Hispania na duniani, baada ya mechi ya Ligi kuu ya wanawake nchini Hispania kati ya wenyeji Atletico Madrid dhidi ya Barcelona kuingiza mashabiki wengi zaidi.

Mchezo huo ambao ulipigwa Jumamosi ya Machi 16, 2019 umevunja rekodi ya mechi ya Ligi ya wanawake kuingiza mashabiki wengi ambayo ilikuwa ni 48,121 kwenye mechi kati ya Athletic Bilbao dhidi ya Ateltico Madrid, kwa kuingiza mashabiki 60,739.

Mchezo huo ulimalizika kwa Barcelona kushinda mabao 2-0 hivyo kupunguza tofauti ya pointi na Atletico ambao wapo kileleni na alama 66 na Barcelona wakiwa nafasi ya pili na pointi 63.