Jumatatu , 17th Dec , 2018

Klabu ya soka ya Yanga kupitia kwa Afisa habari wake Dismas Ten imethibitisha kuwa kocha wa wake Mwinyi Zahera ataondoka nchini muda wowote kuanzia sasa ambapo atakwenda kwenye matibabu nchini Ufaransa.

Kocha Mwinyi Zahera

Dismas amesema hiyo ndio sababu kuu ya mwalimu Zahera kuondoka na sio kama inavyoelezwa kwamba ametofautina na uongozi wa klabu jambo ambalo halina kweli.

''Mwalimu anaondoka na sio jambo geni alishasema mwenyewe mapema kwamba anaweza kukosa mechi moja ya ligi kuu na atarejea wakati wa kombe la mapinduzi kwahiyo sio kweli kwamba anavunja mkataba, ni suala la afya yake tu'', amesema Dismas.

Aidha Dismas ameongeza kuwa matibabu hayo yatakayofanyika Ufaransa yanaratibiwa na shirikisho la soka nchini DR Congo (CAFF), ambalo limemwajiri Mwinyi Zahera kama kocha msaidizi wa timu yao ya taifa.

Baada ya mchezo wa jana dhidi ya Ruvu Shooting, Mwinyi Zahera aliweka wazi kuwa viongozi wa Yanga wamemwangusha kwa kutosajili wachezaji aliowahitaji kwenye dirisha dogo hivyo hatakiwi kuulizwa kuhusu ubingwa.

Dismas pia amesema suala hilo litatolewa ufafanuzi na kamati ya usajili ya Yanga ambayo itaeleza kwanini haikutimiza mahitaji ya mwalimu.