Kikosi cha Mgambo JKT
Ligi Kuu Tanzania bara imeendelea leo katika viwanja vitatu tofauti ambapo Mtibwa Sugar imeendelea kulia baada ya kufungwa na Mgambo Shooting bao 1-0 katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Bao la Mgambo limefungwa na Malimi Busungu dakika ya 27.
Kwa matokeo hayo sasa Mgambo imefikisha pointi 17 na kupanda hadi nafasi ya 12 wakati Mtibwa ikibaki na point zake 19 katika nafasi ya 6.
Ndanda FC ya Mtwara nayo imewachapa Wagosi wa Kaya timu ya Coastal Union kutoka jijini Tanga bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye dimba la Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Ndanda imefikisha point 19 na kupaa hadi nafasi ya 10 wakati Coastal ambayo nayo ina point 19 ikibaki nafasi ya 7.
Huko Shinyanga wakata miwa wa Kagera Sugar wameendelea kuutumia uwanja wa Kambarage kwa mafaniko ambapo leo wamepata ushindi wao wa 3 mfululizo kwa kuwapiga Maafande wa Jeshi la Polisi kutoka mjini Morogoro bao 1-0.
Bao la Kagera limefungwa kunako dakika ya 38 na Rashid Bunda na kuifanya Kagera ifikishe point 24 katika nafasi ya Tatu ikiwa ni point mbili nyuma ya Azam FC.
Polisi Morogoro wamebaki na point zao 19 katika nafasi ya 9.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho Jumapili katika viwanja vitatu tofauti, Uwanja wa Chamazi wenyeji Azam FC wataikaribisha timu ya maafande wa Jeshi la Magereza nchini Tanzania Prisons, mchezo utakaonza majira ya saa 2 kamili usiku.
Mjini Shinyanga wenyeji timu ya Stand United wataikaribisha Simba SC kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku wagonga nyundo wa jiji la Mbeya, timu ya Mbeya City wakicheza na timu ya Young Africans kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.