Jumanne , 28th Aug , 2018

Kufuatia kipigo cha 3-0 kutoka kwa Tottenham Hortspurs usiku wa jana, kocha wa Manchester United, Jose Mourinho ameonesha kutofurahishwa na maswali katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mchezo huo akitaka heshima kutokana na historia yake.

Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho.

Kocha huyo amekumbana na kipigo cha kwanza kikubwa kwenye uwanja wake wa nyumbani katika historia yake ya kufundisha soka huku Spurs ikiandikisha ushindi wa kwanza kwa timu za London tangu Januari 2014 ambapo waliifunga Man United 2-1.

Matokeo yalikuwaje? Ni hivi (akinyoosha vidole vitatu juu). Hii pia ni nini? Premiership tatu, nimeshinda ubingwa wa EPL mara nyingi kuliko makocha 19 wa ligi kwa pamoja, mimi tatu wao mbili, heshima, heshima, heshima “ Amesema kocha huyo na kumalizia kwa maneno “ heshima, heshima, heshima “ huku akiondoka mbele ya wanahabari.

Yawezekana hakufurahishwa na namna ambavyo alikuwa akiulizwa maswali hasa kuhusiana na matokeo ya mchezo huo, ndiyo sababu iliyompelekea kufanya hivyo.

Mourinho aliweka wazi wakati wa maandalizi ya msimu kuwa alitaka kumsajili mlinzi mmoja wa kati lakini bodi ya Manchester United haikutimiza hilo licha ya kuhusishwa juu ya kuwasajili wachezaji kama Harry Maguire wa Leicester City, Toby Alderweireld wa Spurs na Jerome Boateng wa Bayern Munich.

Mashabiki walionekana kutofurahishwa na matokeo hayo na hasa baada ya wachezaji wa Manchester United kukimbilia vyumbani mara baada ya mchezo kwisha, lakini Jose Mourinho aliwasapoti kwa kuwaaga na kuwashukuru kwa uwepo wao.

Kwa matokeo hayo, Manchester United inaungana na kigogo mwingine Arsenal ambao wamepoteza michezo miwili kati ya mitatu ya ligi mpaka sasa, wakiwa na alama tatu pekee.