Mourinho aongelea usajili wa Ozil

Saturday , 2nd Dec , 2017

Kocha wa Manchester United Jose Mourinho amegoma kusema endapo atamsajili au hatomsajili winga wa Arsenal Mesut Ozil, badala yake ameacha mjadala juu ya uhamisho wa nyota huyo ambaye mkataba wake na Arsenal unaelekea mwishoni.

Akiongea na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa ligi kuu soka nchini England leo ambapo timu yake imesafiri hadi London kukabiliana na kikosi cha kocha Arsene Wenger, Mourinho, amesema hana jibu kuhusu suala la usajili wa Ozil.

"Sina majibu kuhusu suala hilo”, alijibu Mourinho alipoulizwa na mwandihsi mmoja kuhusu usajili huo. “Kila mchezaji huwa anaamua kwenda sehemu anayotaka au anayoifurahia kwahiyo siwezi kuongelea hilo”, ameongeza.

Mkataba wa Ozil ndani ya Arsenal unamalizika mwishoni mwa msimu huu wa 2017/18 ambapo mchezaji huyo mwenye miaka 29 ataondoka kama mchezaji huru endapo ataamua kusaini mkataba na Arsenal hadi muda huo.

Nyota huyo raia wa Ujerumani amekuwa akihusishwa na kuhamia klabu za Manchester United pamoja na Barcelona. Mchezaji mwingine ambaye mkataba wake unaelekea ukingoni ndani ya Arsenal ni raia wa Chile Alexis Sanchez.