Jumatatu , 5th Aug , 2019

Menyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba Mohammed Dewji, amesema kuwa ujenzi wa uwanja wa Bunju katika awamu ya kwanza, atagharamikia yeye mwenyewe.

Waziri Mwakyembe akipeana mkono na Mohammed Dewji baada ya kuweka jiwe la msingi.

Mo Dewji amebainisha hilo leo wakati wa uwekaji jiwe la Msingi katika ujenzi huo, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe.

''Mimi kama mwanachama na shabiki wa Simba nimeamua kutoa pesa zangu mfukoni kwaajili ya ujenzi wa awamu ya kwanza ya Bunju Complex, na hizi hazihusiani na zile tulizokubaliana kwenye uwekezaji'', amesema Mo Dewji.

Kwa upande wake Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa wanasimba na vilabu vingine wanatakiwa kuendelea na zoezi la uwekezaji huku kanuni zikiendelea kuandaliwa na hakuna atakayekiuka.

''Timu ya Simba SC waliniomba waendelee nikawakubalia wakati ambao tunatengeneza kanuni na niwahakikishie zitafuatwa na zisitumike kuharibu hamasa, hata kwenye timu zingine karibuni muwekeze'', ameeleza Mwakyembe.

Aidha amewataka wanasimba kuwaunga mkono viongozi wao pamoja na juhudi zote za ujenzi wa uwanja wa Bunju Complex hata kama hawana pesa za kutosha wanaweza kujitolea kwa kazi zinazohitaji nguvu ili kukamilisha jambo hilo la kihistoria.