Alhamisi , 30th Apr , 2015

Mikoa mitano nchini imethibitisha kushiriki ligi ya taifa ya mpira wa kikapu NBL inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Mei nane mpaka 17 mwaka huu uwanja wa ndani wa taifa jijini Dar es salaam.

Akizungumza na East Africa Radio, kamishna wa mipango na ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania TBF, Manase Zabron, amesema walitoa mualiko kwa mikoa mbalimbali nchini ambapo mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Dodoma, Tanga na Mwanza imeshathibitisha ushiriki wa michuano hiyo ambapo ifikapo kesho (Mei 01) utakuwa mwisho wa kuthibitisha ushiriki kwa mikoa iliyobakia.

Manase amesema, Mkoa wa Dar es salaam una jumla ya timu 13 za wanawake na wanaume ambazo ni JKT, Vijana, Savio ABC, Jogoo, Chui, Mabibo, Bullet, Oilers, Pazi, JKT Stars, Jeshi Stars na Don Bosco Lioness.

Manase amesema, mkoa wa Tanga utashirikisha timu za wanawake na wanaume ambazo ni Bandari Tanga, Tanga United na Tanga King's.

Manase amesema, mkoa wa Morogoro utashirikisha timu moja ya wanaume ambayo ni Woriours wakati Dodoma itashirikisha timu mbili ambazo ni Magereza Isanga na UDOM huku ikitarajiwa kuongeza timu moja mabayo ni Planet.

Manase amesema, wanatarajia kuwa na timu 30 katika michuano hiyo ambapo ni 20 za wanaume na 10 za wanawake ambapo bingwa katika michuano hiyo kwa wanaume na wanawake atapata nafasi ya kushiriki michuano ya kanda ya tano itakayofanyika Agosti mwaka huu Kampala nchini Uganda.