Alhamisi , 16th Jul , 2020

Patashika ya ligi kuu Tanzania Bara raundi ya 35 ilieendelea jana kwa mitanange sita kupigwa katika mikoa tofauti hapa nchini.

 

Kiungo wa Yanga Feisal Salum(kushoto katika picha), akipiga shuti mbele ya mshambuliaji wa Azam FC (Kulia katika picha), Idd Kipagwile.

Uwanja wa Majaliwa uliopo mkoani Lindi ,Namungo iliinyuka Mbeya City bao 1-0 lililofungwa na nyota wake Abeid Athuman dakika ya 46 ya mchezo.

Ushindi huo kwa vijana wa kocha Hetimana Thiery umewaimarisha katika nafasi ya 4 katika msimamo wakiwa wamekusanya alama 63 lakini ni kwa Mbeya City ni kipigo kinachowahatarisha zaidi katika nafasi ya kusalia ligi kuu kwani hivi sasa wapo nafasi ya 18 kwa alama 36 huku wakibakia na mechi tatu kumaliza msimu wa 2019/20.

Mchezo mwingine ulipigwa katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo JKT Tanzania ilikipiga na Alliance kutoka Mwanza na mtanange huo ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.

Alliance ambayo inanolewa na kocha Kessy Mziray ilitangulia kupata bao lililosukumiziwa kimiani na David Richard dakika ya lakini maafande wanaonolewa na kocha Mohamed Abdallah Bares walisawazisha dakika ya 90 lililofungwa na Adam Adam .

Kwa matokeo hayo Jkt Tanzania imejiongozea alama moja na kufikisha alama 46 ingawa imporomoka hadi nafasi ya 8 huku Alliance ikifikisha alama 41 katika nafasi ya 14 katika msimamo wa VPL

Katika uwanja wa Kaitaba Kagera Sugar inayonolewa na Mecky Mexime iliifunga Coastal Union ya Tanga kwa bao 1-0 lililofungwa kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Awesu Awesu dakika ya 40 ya mchezo.

Kagera Sugar inasogea hadi nafasi ya 7 ikiwa na alama 46 wakati Coastal Union licha ya kupoteza leo imeendelea kushikilia nafasi ya 5 ikiwa na alama 51 hadi sasa.

Huko Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, Ndanda ya kocha meja mstaafu Abdul Mingange ilikua inajiuliza mbele ya Tanzania Prisons kutoka Mbeya na hadi dakika 90 zikimalizika wanakuchele waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Mabao ya Ndanda yalisukumiziwa kambani na Vitalis Mayanga dk ya 39 na Taro Donald dakika ya 51 huku la kufutia machozi la Prisons likifungwa na Jumanne Elifadhili dakika ya 65 kwa mkwaju wa penati.

Wanakuchele imefikisha alama 40 na kuchupa mpaka nafasi ya 15 wakati Prisons wao wameporomoka kwa nafasi moja hadi ya 11 wakiwa na alama 41.

Mechi nyingine ilichezwa katika uwanja wa CCM Gairo ambapo Mtibwa Sugar ilikua mwenyeji wa Azam FC na matokeo yalikua mazuri kwa kocha Zuberi Katwila baada ya ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Issa Rashid dakika ya 38.

Matokeo hayo yanaisogeza juu ya msimamo Mtibwa kutoka nafasi ya 18 waliyokuwepo mpaka ya 13 wakiwa wamefikisha alama 41 huku kipigo kikiishusha Azam hadi nafasi ya 3 baada ya Yanga iliyocheza usiku dhidi ya Sngida United kushinda kwa mabao 3-1.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Paul Godfrey,Mrisho Ngasa na Yikpe Gislain wakati Singida United wakipata la kufutia machozi kupitia Stephen Sey, sasa wanajangwani wanakwea hadi nafasi ya pili katika msimamo wakiwa na alama 67.

Ligi hiyo itaendelea leo kwa mechi moja kati ya mabingwa Simba watakaowaalika Mbao kutoka jijini Mwanza.