Jumanne , 15th Jan , 2019

Mshambuliaji wa klabu ya Azam FC raia wa Ghana, Enock Atta amefungua njia ambayo ilikuwa ngumu kwa wachezaji wengi wa mataifa ya Magharibi mwa Afrika wanaocheza ligi kuu ya Tanzania kuitwa kwenye timu za Taifa.

Enock Atta Agyei

Klabu ya Azam FC imethibitisha kupokea taarifa kutoka chama cha soka nchini Ghana, juu ya kuitwa kwa Atta kwenye timu ya taifa ya Ghana ya umri chini ya miaka 20 inayokabiliwa na michuano ya AFCON U20.

''Hongera Enock Atta, kwa kuitwa timu ya Taifa ya Ghana chini ya umri wa miaka 20, 'Black Satellite' kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON U-20) zitakazofanyika nchini Niger kuanzia Februari 2 hadi 17 mwaka huu'', imeeleza taarifa ya Azam FC.

Mara nyingi makocha wengi wa mataifa ya Magharibi wamekuwa wakitazama zaidi wachezaji wanaocheza Ulaya lakini uwezo wa kinda huyo aliyesajiliwa Azam FC mwaka 2016 umewashawishi kumjumuisha katika kikosi hicho.