Jumamosi , 26th Nov , 2016

Kiungo chipukizi wa Azam FC, Omar Wayne ameomba kutolewa kwa mkopo timu nyingine ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ili akapate uzoefu zaidi.

Omary Wayne (Mwenye jezi nyeupe)

 

Wayne amesema amejiridhisha kuwa hawezi kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha Azam FC kwa sasa iliyochini ya kocha Mhispania Zeben Hernandez Rodriguez na llengo la kuomba kutolewa kwa mkopo timu nyingine ni ili apate nafasi ya kucheza pamoja na kujikusanyia uzoefu ambao baadaye unaweza kuinufaisha klabu yake hiyo ya Azam FC.

"Mimi ninaomba uongozi unitoe kwa mkopo kwenda timu yoyote ili nipate nafasi ya kucheza, nipate uzoefu ili na mimi nikuze uwezo wangu kuliko hivi ninavyokaa Azam bila kucheza", amesema Wayne.

Wayne amesema anaamini akitolewa kwa mkopo kwenda timu nyingine ya Ligi Kuu atapambana kugombea namba na kupata nafasi ya kucheza.

Wayne amesema, Azam FC ina wachezaji wengi kuanzia timu ya vijana hadi timu ya wakubwa na ushindani pia ni mkubwa hivyo inakuwa ngumu kwa wachezaji wengi wadogo kupata nafasi.

“Nina matumaini makubwa nikipata nafasi ya kucheza siku moja nitarudi Azam kishujaa kwa sababu naamini uwezo wangu na ndiyo maana napigania kutolewa kwa mkopo,”amesema Wayne.

Omary Wayne alikuwa nahodha wa kikosi timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys mwaka 2014 wakati huo akiwa na kikosi cha timu ya vijana ya Azam FC ambapo mwaka jana alitolewa kwa mkopo kwenda Majimaji na baadaye African Sports ya Tanga kabla ya Julai mwaka huu kuitwa kwa majaribio timu ya Amazulu inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini, ambako pamoja na kufuzu, lakini klabu hiyo haikuwa tayari kuvunja mkataba wake na Azam FC.