Jumanne , 13th Nov , 2018

Klabu ya soka ya Mbao FC imetajwa miongoni mwa timu 4 zitakazoshiriki michuano ya Sports Pesa Super Cup 2019, itakayofanyika jijini Dar es salaam.

Kikosi cha Mbao FC

Akiongea na wanahabari leo Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa Sport Pesa Tanzania Tarimba Abbas, amesema wameyarejesha mashindano hayo nchini baada ya msimu uliopita kufanyika nchini Kenya.

''Msimu wa tatu wa michuano hii tumeona urudi Tanzania kutokana na hamasa ya mashabiki na kwasababu hiyo tumeongeza timu moja ziwe 4 badala ya 3 zilizoshiriki msimu uliopita kwa kuwapa nafasi Mbao FC ya Mwanza'', amesema.

Timu nyingine za Tanzania zimeendelea kuwa zilezile tatu ambazo ni Simba SC, Yanga SC na Singida United. Msimu uliopita Yanga ilitolewa hatua ya awali kabla ya Singida United kutolewa nusu fainali na Simba ikifungwa fainali na Gor Mahia.

Kwa upande mwingine Tarimba amezitaja timu za Kenya kuwa ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo Gor Mahia, Kariobangi Sharks Bandari FC na AFC Leopards.