Jumatatu , 14th Nov , 2022

Uongozi wa Klabu ya Simba umethibitisha kuwa Kocha wao Msaidizi wa Simba, Seleman Matola ataondoka kwenye benchi la ufundi la timu hiyo kwa muda kwaajili ya kwenda kwenye kozi ya Ualimu ya leseni A ya CAF, itakayoanza Novemba 21 mwaka huu.

Taarifa hiyo imethibitishwa na Meneja wa Mawasiliano Simba SC, Ahmedy Ally ambaye amesema, wanafurahi kwa hatua hiyo kwani Matola akiimaliza kozi hiyo basi atakuwa atapanda daraja na kuruhusiwa kuwa Kocha Mkuu katika vilabu vya Ligi kuu.

''Ni kweli tumepokea maombi kutoka kwake na hii ni fursa kwake kwenda kujiongeza katika idara ya elimu , sisi Simba tunamtakia kila la kheri'' amesema Ahmedy Ally.

Mabosi wa Simba watalazimika sasa kuboresha benchi la ufundi kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma kocha huyo alipokwenda kusoma timu ikiwa chini ya Didier Gomes ambapo alitafutiwa msaidizi wake Thierry Hitimana na baadaye Matola aliungana nao alipomaliza masomo yake.

Simba inatarajiwa kushuka dimbani Jumatano ya Novemba 16 mwaka huu kucheza mchezo wa Ligi Kuu NBC Tanzania dhidi ya Namungo katika uwanjna wa Benjamin Mkapa majira ya saa moja usiku .