Jumanne , 15th Jun , 2021

Mlinzi wa kati wa timu ya taifa ya Hispania Aymeric Laporte amkingia kifua mshambuliaji wa timu hiyo Alvaro Morata kwa kukosa mabao kwenye mchezo wa Euro 2020 dhidi ya Sweden mchezo ambao ulimalizika kwa suluhu (0-0).

Morata

Mwishoni mwa mchezo huo mashabiki walimpigia miluzi na kumzomea Morata kutoka na kukosa nafasi kadhaa za kufunga mabao ambazo alizipata kwenye mchezo huo.

''Kuzomewa sio jambo jipya, huwezi kuwa na wasiwasi na mshambuliaji kama Alvaro Morata ambaye ameshaonyesha vitu vingi. Ni kweli hakuwa na usiku mzuri lakini kwenye michezo ijayo atawaziba midomo, tumekosa magoli leo lakini siku moja tutafunga matano na siku nyingine hatutafunga.'' amesema Aymeric Laporte

Sio mara ya kwanza kwa Morata kuzomewa kutokana na kushindwa kutumia vizuri nafasi za kufunga mabao, mshambuliaji huyo anayekipa katika klabu ya Juventus ya Italia ameshaichezea Hispania jumla ya michezo 41 na amefunga jumla ya mabao 19.

Hispania ambao ni mabingwa mara tatu wa michuano ya Euro pia kwenye mchezo huo imeweka rekodi, kwenye dakika 45 za kipindi cha kwanza timu hiyo ilipiga pasi 419, ikiwa ni idadi kubwa tangu mwaka 1980, lakini pia timu hiyo ilipiga mashuti 17 yakiwa ni mengi zaidi katika historia ya timu hiyo kwenye mashindano makubwa iwe kwenye Euro au Kombe la Dunia.

Sasa Hispania inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi E, ambapo timu ya taifa ya Slovakia ndio inayoongoza kundi hilo ikiwa na alama 3 ilizozipa baada ya kuifunga Poland mabao 2-1.