
Kesho Jumatano FIFA itakuwa na agenda namba 13 kwenye mkutano wake Mkuu wa 68, ambayo ni kupiga kura ya kuchagua taifa mwenyeji wa Kombe la Dunia 2026 ambalo kwa mara ya kwanza litashirikisha timu 48. Mataifa yaliyoomba ridhaa hiyo ni Canada, Mexico, Marekani na Morocco.
Marekani imeomba kushirikiana kwa pamoja na nchi za Canada pamoja na Mexico ambapo viwanja zaidi ya 16 katika mataifa hayo vitatumika kuandaa fainali hizo. Viwanja 10 nchini Marekani na vinne Mexico na Canada. Huku fainali ikitarajiwa kupigwa MetLife (84,953), jijini New York.
Morocco yenyewe ipo tayari kutumia viwanja 14 kuandaa fainali hizo ambapo mchezo wa fainali utapigwa uwanja wa Grand Stade de Casablanca (93,000). Tayari kuna viwanja 8 vyenye sifa na vingine 6 vitajengwa endapo watapata uenyeji. Kwa upande wa Morocco huenda ikapata kura ya mataifa ya Ulaya kutokana na nchi nyingi za Ulaya kupakana na Morocco.
Kura ya kuamua itapigwa na mataifa wananchama wa FIFA ambayo ni 211 lakini mataifa yaliyoomba ambayo ni Canada, Mexico Marekani na Morocco hayatapiga hivyo kura zitakazopigwa ni 207. Endapo Morocco atashinda Fainali hizo zitaandaliwa Africa kwa mara ya pili baada ya 2010 nchini Africa Kusini.