Alhamisi , 15th Aug , 2019

Afisa Habari wa Klabu ya Simba, Haji Manara amesema kuwa amejitolea kuwasapoti wapinzani wake Yanga, Azam FC na KMC katika michezo ya Kimataifa kwa kuwa ni suala la Kitaifa.

Haji Manara

Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Makao Makuu ya TFF leo, Manara amesema kuwa linapokuja suala la Kitaifa huwa anaacha unazi wa klabu yake na kuungana, hivyo yuko tayari kusapoti timu hizo ili kwa pamoja zifuzu hatua ya makundi ya michuano ya vilabu Afrika, akihofia kuwa kufeli kufanya vizuri kwa timu hizo kutarudisha nyuma nafasi nne walizozipata katika miaka ijayo.

"Siwapendi kwelikweli Yanga lakini kwenye masuala ya Kitaifa, dua na sala zangu naelekeza kwao lakini wao huwa hawanielewi. Wakifungwa nitawacheka sikatai lakini kwa sasa ninawaombea wote sisi tufuzu hatua ya makundi kuna faida nyingi sana, na sio Simba tu na Yanga bali hata Azam na KMC", amesema Manara.

Aidha Manara amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa Ngao ya Jamii Jumamosi hii kati ya Simba na Azam FC katika Uwanja wa Taifa.