Jumanne , 20th Aug , 2019

Klabu ya Manchester United imeeleza kusikitishwa na kauli za kibaguzi za mashabiki wa klabu hiyo zinazoelekzwa kwa kiungo wake Paul Pogba kufuatia kukosa penalti katika mchezo wa ligi dhidi ya Wolves.

Paul Pogba na Marcus Rashford

Katika mchezo huo, Pogba alikosa penalti katika dakika ya 68 ya mchezo, ambapo mwisho wa mchezo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Sehemu ya taarifa iliyotolewa na Manchester United kuhusu suala hilo imesema, "kila mmoja hapa Mmanchester United amesikitishwa na ubaguzi unaoendelea juu ya Paul Pogba kwa kilichotokea usiku wa jana, tunlaani kwa nguvu kitendo hicho".

"Yoyote anayefanya kitendo hiki hawakilishi thamani na ukubwa wa klabu yetu na inatia faraja kuona mashabiki wakilaani suala hili katika mitandao ya kijamii. Tunafanyia kazi kuwafahamu wachache waliohusika katika suala hilo na kuwachukulia hatua kali. Pia tunahimiza makampuni ya mitandao ya kijamii kuchukua hatua kwenye hili", imeendelea kusema taarifa hilo.

Man United ina alama nne mpaka sasa katika michezo miwili iliyocheza, ikishinda mchezo wa kwanza dhidi ya Chelsea na kutoka sare mchezo wa pili dhidi ya Wolves, Jumatatu Agosti 19.