Jumanne , 15th Nov , 2022

Jumla ya mabondia 30 wamefanikiwa kupima  afya tayari kwa maandalizi ya mwisho  kuelekea pambano la Dar Boxing Derby linalotarajia kupigwa Novemba 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kinesi, Dar

Mabondia hao watacheza pambano hilo akiwemo Ally Ngwando wa Manzese ambaye anatarajia kucheza pambano kuu ‘main card; dhidi ya Ismail Boyka kutoka Gongo la Mboto, Dar huku kiingilio katika pambano hilo kikiwa ni Sh 5000 kabla na Sh 10,000 mlangoni huku Sh 15000 ikiwa ni kwa VIP.

Mratibu wa pambano hilo, Bakari Khatibu alisema kuwa wamekamilisha zoezi la kwanza kwa upimaji afya za mabondia kuelekea kwenye pambano hilo ambalo linasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa mchezo huo.

“Tayari leo tukiwa kama waandaji tumekamilisha sehemu ya kwanza ya maandalizi kwa kuwapima afya mabondia wote kutokana na kanuni na sheria za mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini.

“Kitu kikubwa ambacho tunataka kuwaambia mashabiki tukiw kama waandaji tumekuwa tukifanya mambo kwa utofauti mkubwa kwa sababu wasitegemee kuona Uwanja wa Kinesi kuwa unavyokuwa kwenye mapambano mengine, tumejipanga kuleta utofauti na hata wale ambao watakuwa wamekata tiketi za VIP basi watapata hadhi ya kuwa katika VIP,” alisema Khatibu.

Miongoni mwa mabondia waliopima afya ni Karimu Mandonga ambaye amewataka mashabiki wa mchezo huo kujitokeza kwa wingi katika pambano hilo la Dar Boxing Derby huku akisisitiza kuwepo kwa ngumi yake ya ndoinge kwenye pambano hilo.

“Tayari tumekamilisha zoezi la kupima afya kwa ajili ya maandalizi ya pambano la Dar Boxing Derby na jambo kuwa ni kuhamasisha wadogo zetu hiyo siku mashabiki wanataka kushuhudia ngumi hasa yaani watu wapigane mpaka Yesu azaliwe tena na ngumi ndoige zionyeshwe,”.

Kwa upande wa upande wa daktari aliyesimamia zoezi hilo, Khadija Hamisi alisema kuwa kawaida wamekuwa wakisimamia kuwapima magonjwa matatu kabla ya kupanda ulingoni ambapo aliyataja magonjwa hayo ni homa ya ini, kisukuri na ukimwi.

Mabondia wengine watakaopanda ulingoni kwenye pambano hilo ni Gilbert Machupa dhidi ya Juma Kichupa, Joseph Maigwisa na Ibrahim Tamba lakini Mudy Pesa akitarajia kucheza na Man Chuga huku Yuko Kyando akipewa kucheza na Hemedi Rashid.

Wengine ni Vigulo Shafii na Bakari Dunda, Hamad Furahisha dhidi ya Max Mushi, Paul Magesta na Haruna Ndaro, Emmanuel Kitimtim na Swahibu Ramadhan wakati Mshamu Mohamed atacheza na James Killian huku Peter Tosh akipewa kuzima na Jackson Malinyingi.