Jumamosi , 17th Dec , 2016

Baada ya mapumziko ya muda wa mwezi mmoja, michuano ya Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara mzunguko wa lala salama unaendea hii leo, ambapo mabingwa watetezi Yanga chini ya kocha mpya George Lwandamina wataanza dhidi ya JKT Ruvu Stars uwanja wa Uhuru DSM.

Kocha mpya wa Yanga George Lwandamina

Baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 33, wakizidiwa pointi mbili na vinara Simba SC, yanga walibadilisha benchi la Ufundi ambapo aliyekuwa Kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm amekuwa Mkurugenzi wa Ufundi, na nafasi yake akimuachia Mzambia, George Lwandamina.

Mechi nyingine za Ligi Kuu leo ni Mbeya City watamenyana na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Mwadui dhidi ya Toto Africans uwanja wa Mwadui Complex Shinyanga, na Ruvu Shooting akicheza dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.

Vinara wa ligi hiyo, Simba watashuka dimba la Nangwanda sijaona Mtwara hapo kesho kumenyana na Ndanda FC, wakati Mbao FC watamenyana na Stand United Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, African Lyon na Azam Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na Prisons atacheza dhidi ya Maji Maji Uwanja wa Sokoine, Mbeya.