Ijumaa , 18th Sep , 2015

Michuano ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania bara inatarajiwa kuendelea hapo kesho katika mzunguko wake wa tatu katika viwanja vinne nchini huku timu nane zikitarajiwa kuchuana kusaka pointi tatu muhimu.

Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, mabingwa watetezi wa Kombe hilo Dar es salaam Young African watashuka kumenyana na JKT Ruvu huku jijini Mbeya vumbi likitimka kwa kuwakutanisha watani wa jiji hilo wajelajela Tanzania Prisons dhidi ya mbeya City.

Uwanja wa Kambarage Mjini Shinyanga utawakutanisha Stand United wakiwakaribisha African Sports huku uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga Mgambo Shooting wakiwakaribisha Majimaji FC ya mjini Songea.

Mzunguko wa tatu wa ligi hiyo utamalizika hapo Jumapili kwa mechi nyingine nne kupigwa ambapo wekundu wa Msimbazi Simba wakishuka dimbani dhidi ya Kagera Sugar huku wanarambaramba Azam FC wakiwa ugenini Uwanja wa Mwadui mjini Shinyanga wakicheza dhidi yaMwadui FC.

Uwanja huku Manungu Mkoani Morogoro Mtibwa Sugar watawakaribisha Ndanda FC ya Mjini Mtwara huku mzunguko huo ukikamilishwa na wagosi wa Kaya Coastal Union ya Jijini Tanga wakishuka dimbani kuwakaribisha Toto Africans ya jijini Mwanza Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.