Jumatano , 25th Dec , 2019

Yanga imecheza mchezo wa ligi jana Jumanne, Disemba 24 dhidi ya Mbeya City katika uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.

Kocha Boniface Mkwasa

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bila kufungana na baada ya mchezo kumalizika, makocha walipata nafasi ya kuzungumzia mchezo huo ambapo kocha wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa alionekana mwenye jazba na kutupa lawama nyingi kwa waamuzi, akiwaita kuwa ni kichefuchefu.

"Mchezaji yupo karibu na mwamuzi, kuna matukio fulani yanatokea lakini waamuzi wanakuwa hawatendi haki. Waamuzi kama hawa ni kichefuchefu, hatuwezi kuwalaumu lakini wanaharibu ligi na hatuwezi kufika popote kama ni hivi", amesema Mkwasa.

Naye kwa upande wake kocha wa Mbeya City, Amri Said amezungumzia kiufundi namna walivyofeli kuibuka na ushindi pamoja na mapungufu ya kikosi chake.

"Kitu kikubwa nilikuwa nakifanya kwa wachezaji kwanza ni kutengeneza saikolojia ya wachezaji wangu, pia nilikuwa nafundisha spidi na ufundi ukizingatia wachezaji wa Yanga wana maumbo makubwa hivyo nilihitaji wachezaji wangu wawe haraka kupokonya mipira na kuondoka", amesema Amri Said.

Kutokana na kauli za makocha wote wawili kuna utofauti wa namna ya uzungumzaji wao, kocha wa Yanga huenda alitegemea kupata matokeo mazuri kwa asilimia kubwa bila kuangalia pia uwezo wa Mbeya City lakini kocha wa Mbeya City aliingia na mbinu ambayo hata pointi moja aliyoipata ameonekana kuifurahia.

Yanga hivi sasa ina pointi 18 baada ya kushuka dimbani michezo tisa ya ligi huku ikiwa katika nafasi ya tisa. Mbeya City imeongeza pointi moja na kufikisha pointi tisa baada ya kucheza michezo 13 huku ikiwa katika nafasi ya 18 ya msimamo.