Jumatatu , 21st Jul , 2014

Kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa ya vijana ya Tanzania ya umri chini ya miaka 17 Serengeti Boys Hababuu Ally ameiomba TFF ihakikishe vijana wake wanaweka kambi ya mapema katika mji au mkoa ambao hali ya hewa inalingana na Afrika kusini

Wachezaji wa timu za Serengeti boys na Amajambos wakipeana mikono kabla ya mchezo wao wa juzi.

Timu ya soka ya taifa ya vijana ya Tanzania umri chini ya miaka 17 Serengeti Boys inataraji kuingia kambini kesho mara baada ya kumaliza siku tatu za mapumziko walizoanza Ijumaa mara baada ya kutoka sare ya 0-0 na Amajamboz ya Afrika Kusini katika mchezo wa kwanza wa hatua ya pili ya kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Afrika kwa vijana itakayofanyika mwakani nchini Niger

Kocha mkuu wa timu hiyo Hababuu Ally amesema baada ya kuona mapungufu katika mchezo huo ambao ulipigwa katika uwanja wa chamazi amepeleka pendekezo kwa TFF ili kuhakikisha timu hiyo inakwenda Afrika kusini mapema na pia inaweka kambi katika eneo ambalo hali ya hewa inalingana na Afrika kusini ili afanye maandalizi ya kutosha kwaajili ya mchezo wa marudiano

Hababuu ambaye ameahidi kuyafanyika kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo huo wa juzi amesema baada ya kufanya mawasiliano na baadhi ya marafiki zake walioko nchini Afrika kusini wamemwambia kuwa hali ya hewa kwa baadhi ya miji ni baridi sana na hivyo yeye ameamua kutoa taarifa mapema kwa TFF ili timu hiyo iweze kuweka kambi katika miji kati ya Tukuyu au Lushoto na amependekeza timu hiyo iende mapema nchini Afrika kusini ili wachezaji wazoee hali ya hewa ya mji ambao watachezea mchezo huo wa marudiano.