Ijumaa , 11th Sep , 2015

Kivumbi cha ligi kuu ya soka Tanzania Bara 2015/2016 kinatarajiwa kuanza hapo kesho kwa mechi saba kupigwa katika viwanja saba hapa nchini huku mchezo mmoja ukipigwa Jumapili uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Katika michuano hiyo inayoshirikisha timu 16, klabu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera itatumia uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora kwa mechi zake za nyumbani ili kupisha shughuli za uwekaji nyasi bandia inayoendelea kwenye uwanja wao wa Kaitaba mjini Bukoba.

Katika michuano hiyo hapo kesho, Ndanda FC ya Mtwara itawakaribisha Mgambo Shooting katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, African Sports watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku Majimaji wakiwa wenyeji wa maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Azam FC watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons katika uwanja wa Chamazi Complex, Stand United FC chama la wana watawakaribisha Mtibwa Sugar katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Toto Africans watawakaribisha Mwadui FC uwanja wa CCM Kirumba na Mbeya City watacheza na Kagera Sugar katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Jumapili ligi hiyo itaendelea kwa mchezo mmoja utakaochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ambapo mabingwa watetezi wa kombe hilo Yanga SC watawakaribisha wagosi wa kaya Coastal Union.