
Mwanariadha wa Kenya, Eliud Kipchoge
Kipchoge, ambaye anachukuliwa kama mwanariadha bora wa wakati wote, anakuwa mwanariadha wa tatu kushinda mara mbili mbio za marathoni katika Olimpiki, na alimaliza mbio hizo za Tokyo 2020 kwa kutumia muda wa saa mbili dakika nane na sekunde 38.
“Nadhani kwa kushinda marathoni mara mbili mfululizo nimefanikiwa kuweka alama na urithi, sasa nategemea itasaidia kuhamasisha kizazi kijacho,” alisema Kipchoge akiongea na vyombo vya habari vya kimataifa.
Kufuatia ushindi wa mwanaridha huyo maarufu, mitandao ya kijamii nchini Kenya imejaa pongezi kwa Kipchoge huku wakipendekeza kwa Rais Uhuru Kenyatta kumjengea sanamu mwanariadha huyo kutokana na heshima aliyoiletea nchi hiyo na Afrika kwa jumla.