Jumamosi , 14th Jul , 2018

Nyota mpya wa klabu ya soka ya KMC inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni, Abdulalim Humud, amesema lengo la timu hiyo si kuwa na majina makubwa tu bali ni wachezaji kuwa na msaada katika kutimiza malengo ya timu.

Mchezaji Abdulhalim Humud

Humud ameyasema hayo leo kwenye mahojiano na www.eatv.tv ambapo ameweka wazi kuwa licha ya timu hiyo iliyopanda kucheza ligi kuu msimu wa 2018/19 kusajili wachezaji wakongwe lakini suala la muhimu ni wachezaji hao kwa kushirikiana na wengine kuhakikisha mipango ya timu inatimia.

''Siamini katika majina makubwa tu pekee, naamini katika wachezaji wanaoweza kuisaidia KMC, uongozi umefikiria watu wenye uzoefu lakini kikubwa ni namna gani watahakikisha timu inamaliza katika nafasi iliyosalaa kwenye msimamo wa ligi'', amesema.

KMC imesajili wachezaji wenye uzoefu mkubwa kwenye ligi kuu soka Tanzania bara pamoja na ligi mbalimbali nje ya Tanzania kama mlinda mlango Juma Kaseja na mshambuliaji Elias Maguli.

Kwa upande wake Humud amewahi kuzichezea klabu tofauti za Tanzania zikiwemo Simba na Azam FC kabla ya kwenda nchini Oman na Afrika Kusini. KMC ni miongoni mwa timu 6 zilizopanda kucheza ligi kuu msimu huu na tayari imeshaonekana kufanya maandalizi mazuri.