Hitimana Thiery kutua Simba?

Ijumaa , 10th Sep , 2021

Uongozi wa Klabu ya Mtibwa Sugar umeshindwa kuthibitisha taarifa zinazomuhusisha Mkufunzi wao Thiery Hitimana kujiunga na Mabingwa wa Nchi, Simba SC baada ya kukosekana asubuhi ya leo katika uwanja wa mazoezi.

Thiery Hitimana

Afisa Habari wa wakatamiwa hao, Thobius Kifaru Ligalambwike ameiambia East Afrika Radio kuwa anahitaji kupata taarifa kam,ili kutoka kwa Mwanasheria wao kabla ya kutolea ufafanuzi juu ya ajira ya Mrwanda huyo aliyewahi kuifundisha Namungo.

Taarifa hizo zinakuja muda mchache kufuatia ripoti zinazoonyesha kuwa huenda Simba ikamchukua Hitimana kwa muda ambaye atafanya kazi badala ya Didier Gomes anayetajwa kutokidhi vigezo vya leseni kwa mujibu wa Shirikisho la soka Afrika CAF. Katika hatua nyingine Uongozi wa Klabu ya Mtibwa umeweka wazi kuwa wamefanya usajili wa viwango vya juu kwa kuleta wachezaji wenye uzoefu ili kuondokana na adha ya kutaka kushuka daraja waliyokutana nayo miaka ya nyuma.

Tobias kifaru amesema kuwa baada ya Uongozi wa timu kubaini changamoto hiyo waliaamua kuongeza wachezaji wakongwe na wenye uzoefu wa ligi yetu pamoja na kupandisha vijana wanne kutoka kwenye timu yao ya vijana iliyotwaa ubingwa msimu uliopita.

Amechagiza kuwa uwepo wa wachezaji kama Ibrahim Ame, Abdi Banda pamoja na Said Ndemla ndani ya kikosi chao utaleta faida na msaada mkubwa kuwapatia uzoefu wachezaji wengine pamoja na wale wadogo waliopandishwa kutoka timu B na kumpunguzia kazi Kocha wao,Pia uwepo wao ndani ya mtibwa utawasaidia kurejea ndani ya timu ya Taifa ya Tanzania pamoja na kupata nafasi ya kucheza soka nje ya Tanzania.