Jumanne , 8th Jan , 2019

Kocha mkuu wa mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania Bara, Patrick Aussems amesema ni bahati mbaya kumkosa mlinzi wake Erasto Nyoni kwenye mechi dhidi ya JS Souara Jumamosi hii.

Patrick Aussems

Akiongea visiwani Zanzibar leo kuelekea mchezo wa Simba dhidi ya Mlandege, katika michuano ya Mapinduzi, Aussems amesema ni pigo kumkosa kiraka huyo lakini anao wachezaji wa kutosha.

"Ni bahati mbaya Erasto Nyoni atakuwa nje ya uwanja kwa takribani wiki tano, hivyo ndio mchezo wa soka ulivyo unaweza kumhitaji mchezaji muhimu kwenye mchezo muhimu lakini ukamkosa'', amesema.

Hata hivyo Aussems amekiri kuwa atafanyia kazi pengo hilo kwa kuwatumia wachezaji wengine kwenye kikosi chake na tayari ameshawaandaa kwaajili ya hilo.

Nyoni aliumia goti la kulia kwenye mchezo wa Mapinduzi Cup dhidi ya KMKM, juzi usiku ambapo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.