Jumanne , 21st Jun , 2022

Kocha Msaidizi wa klabu ya Yanga raia wa Burundi Cedric Kaze amesema Yanga haiwezi kurudia makosa yaliyojitokeza mwanzoni mwa msimu uliopita ya kusajili wachezaji na kushindwa kupata vibali vya kufanyia kazi kwa wachezaji nchini (ITC).

Kocha Msaidizi wa klabu ya Yanga raia wa Burundi Cedric Kaze

Akiongea na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Yanga dhidi ya Polisi Tanzania Kaze amebainisha kuwa viongozi wa klabu hiyo wanaendelea na jitihada za kuhakikisha wanakamilisha usajili wa wachezaji waliopendekezwa na benchi la ufundi kwa ajili ya kuimarisha kikosi hicho.

'' Tumepokea barua kutoka CAF kuhusu kusogezwa mbele kwa tarehe ya kuanza kwa michezo ya hatua ya awali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afika kwa msimu 2022/2023'' amesema Kaze.

Katika hatua nyingine,Kaze amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi hapo kesho huku kikosi hicho kikitarajiwa kukosa huduma ya nyota wawili nahodha Bakari Mwamnyeto na Djuma Shabaan kutokana na kutokuwa na utimamu wa mchezo kwa asilimia mia moja.

Yanga imekata tiketi ya kushiriki ligi ya mabingwa barani afrika baada ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania kwa msimu 2021/22 huku wakitarajiwa kukabidhiwa kombe lao mnamo Juni 25 kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City utakaofanyika jumamosi,Jijini Mbeya