Mwinyi Zahera
Akiongea na EATV & EA Radio Digital moja kwa moja kutoka DR Congo, Zahera amesema yeye anarudi kuendelea na kazi yake Yanga na sio kweli kwamba hataki kurudi kwasababu anadai mshahara bali alikuwa na ruhusa ya mapumziko ya siku 15.
''Ingekua kama mimi sirudi Yanga mwenyewe ningesema, maisha yangu hayategemei mshahara nina biashara zangu na nimeajiri watu 42 DR Congo na wanne huko Ulaya, kwahiyo nina maisha nje ya kufundisha'', amesema.
Aidha Zahera ameongeza kuwa yeye binafsi anaweza kuishi kwa kufundisha timu hata tatu tofauti bila kulipwa na bado maisha yake yakaendelea vizuri.
Zahera ameeleza kuwa baada ya mapumziko ya siku 15 barani Ulaya, atarejea kuendelea na kazi yake ya Yanga na atawahi kujiunga na timu kabla ya mechi yao ya Wiki ya wananchi ambayo itapigwa Agosti 4 dhidi ya Kariobang Sharks ya Kenya.

