Jumatano , 13th Oct , 2021

Timu ya Taifa ya Denmark imekuwa timu ya pili baada ya Ujerumani kufuzu fainali za kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Qatar baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Austria.

Nyota wa Denmark wakishangilia ushindi

Bao pekee lililofanikisha mchakato huo lilifungwa na beki wa Klabu ya Atalanta, Joakim Maehle dakika ya 23 ya mchezo na kupeleka furaha kwa wakazi wa Denmark katika usiku wa jana.

Kikosi cha Denmark kimekuwa na stori ya kushangaza mwaka huu ambapo kupitia michuano ya ya mataifa ya Ulaya, walifanikiwa kutinga nusu fainali, licha ya safari yao kugubikwa na tukio la kiungo wake Christian Eriksen kuanguka uwanjani kwenye moja ya mchezo.

Rekodi ya kuvutia kwa kikosi hicho chenye mseto wa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa katika vilabu vya Ulaya, wamefuzu kibabe kwa kushinda mechi 8, wakifunga mabao 27 huku wakiwa hawajaruhusu bao hata moja.

Denmark inarejea kwenye Kombe la Dunia kwa mara ya 6 ili kujaribu kufanya vyema zaidi ya hatua ya 16 bora ambayo walikwamia mwaka 2018 walipotupwa nje na wana fainali mwaka huo Croatia.

Mafanikio makubwa kwa Denmark kwenye fainali za kombe la Dunia ilikuwa mwaka 1998 walipotinga hadi robo fainali.