Jumatatu , 3rd Mei , 2021

Kocha wa Inter Milan ya Italia, Antonio Conte amefunguka na kusema, siri ya kubeba ubingwa wa ligi kuu nchini humo ni malipo ya kamari waliyoifanya pamoja na Uongozi wa klabu hiyo wakati wanamsajili.

Kocha wa Inter Milan, Antonio Conte (kwenye picha ndogo) na mmiliki wa klabu hiyo, Steve Zhang.

Conte ameyasema hayo ikiwa ni usiku mmoja tu umepita baada ya kuthibitishwa kuwa mabingwa wapya wa Serie A kwa mara ya kwanza tokea mwaka 2010 na kupindua ufalme wa Juventus wa kutwaa taji hilo mara tisa mfululizo na mara tatu ikiwa chini ya Conte mwenyewe.

Akielezea furaha yake baada ya ubingwa huo, Conte amesema, “Haya ni moja ya mafanikio muhimu kwenye maisha yangu ya ukocha, Kujiunga na Inter Milan haikuwa rahisi, ni kipindi ambacho timu haikuwa tayari kushinda mataji kwa haraka”.

“Mbaya zaidi mpinzani ni Juventus ambaye nilifanya naye kazi kwa muda mrefu ambaye ametawala kwa miaka tisa. Leo tunaweza kusema kamari yetu imelipa”.

Ikumbukwe kuwa, Inter Milan ilipopoteza fainali ya kombe la ligi ya EUROPA kwa maba0 4-2 dhidi ya Seville msimu uliopita, hatma ya Koch ahuyo kusalia na miamba hiyo ya Italia ilikuwa na utata, lakini Conte alikwepa kujibia hatma yake ya moja kwa moja klabuni hapo.

Conte amesema, “Tumefanya kitu kikubwa sana na nataka kufurahia wakati huu” maneno ambayo hayajathibitisha kama mkali huyo aliyebeba Serie A kwa mara ya nne kusalia Inter Milan kwa muda mrefu licha ya kubakisha miezi 12 kwenye mkataba wake wa sasa.

Inter Milan imethibitishwa kuwa bingwa usiku wa kuamkia leo baada ya Atalanta kutoka sare ya 1-1 na Sassuolo na Atalanta kufikisha alama 69, Inter akiwa na alama 82 baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Crotone siku ya Jumamosi ya Mei 1, 2021 alam aambazo haziwezi kufikiwa.

Inter imetwaa ubingwa na kuweka rekodi kadhaa, ikiwa bingwa wa kwanza kucheza michezo 18 ya ungwe ya pili bila kufungwa na kumaliza ligi akiwa na safu bora ya ulinzi kwa kuruhusu mabao 29 kwenye michezo 34 licha ya michezo mine kusalia.