Jumamosi , 17th Feb , 2018

Klabu ya soka ya Yanga ambayo inaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Afrika inatarajia kuondoka nchini kesho kwenda Shelisheli huku nyota wake Obrey Chirwa akiachwa nje ya kikosi.

Akiongea na waandishi wa habari leo afisa habari wa Yanga Dismas Ten amesema maandalizi ya safari hiyo yamekamilika na timu itasafiri na nyota 20 lakini Chirwa atakosekana.

''Yanga SC inatarajia kusafiri kesho asubuhi kueleka Shelisheli tayari kwa mchezo wa marejeano na wenyeji  St. Louis FC kwenye ligi ya mabingwa Afrika mchezo uliopangwa kuchezwa jumatano ijayo Stade Liete'', amesema.

Ten ameongeza kuwa jumla ya nyota 20 na viongozi 10 kati yao 8 kutoka benchi la ufundi watasafiri lakini mshambuliaji Obrey Chirwa hatakuwepo kwenye kikosi hicho kwasababu ya maumivu ya misuli aliyopata kwenye mchezo dhidi ya Majiamaji.

Pia kiungo Thabani Kamusoko ambaye amepona majeraha yake hivi karibuni na kuanza mazoezi mepesi pia ameondolewa kwenye orodha ya nyota ambao wangesafiri kuelekea Shelisheli ili apate muda wa kujifua zaidi kurejesha makali yake.