Jumanne , 28th Aug , 2018

Nchi ya Cameroon huenda isiwe katika nafasi nzuri ya kuandaa michuano mataifa ya Afrika AFCON mwakani kama mwenyeji baada ya mchakato wa maandalizi kutokwenda inavyotakiwa mpaka sasa huku miezi michache ikiwa imebakia.

Timu ya taifa ya Cameroon ilipochukua ubingwa wa AFCON 2017.

Akizungumzia kuhusu maandalizi ya michuano hiyo, Rais wa shirikisho la soka barani Afrika CAF, Ahmad Ahmad amesema.

“Sina uhakika kama Cameroon wako tayari kuandaa AFCON, kuna vitu vingi sana ambavyo bado havijakamilika na mpaka sasa kuna muda mchache sana umebakia“.

“Itakuwa ni hatari kuwachezesha wachezaji wetu wa kimataifa hasa wale wanaocheza Ulaya na mabara mengine katika mazingira magumu na  yenye miundombinu mibovu. Kama hauko tayari ni bora utoke na useme kuwa hauko tayari kuandaa“. Ameongeza Ahmad Ahmad.

Ahmad Ahmad pia ameitaja miundombinu ya viwanja na hoteli kuwa ni tatizo kubwa ambalo bado haliko sawa kwa mabingwa hao wa kihistoria mara tano wa michuano ya AFCON.

Michuano hiyo inatarajia kuanza 7 hadi 30 Juni mwaka 2019 huku ikihusisha timu 24, ikiwa ni ongezeko la timu nane kwa mara ya kwanza kutoka timu 16 AFCON iliyopita. Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais wa shirikisho la soka la Morocco, Fouzi Lekjaa alihusishwa na tetesi kuwa nchi yake inapanga kuchukua nafasi ya Cameroon kuandaa michuano hiyo kama mwenyeji.

Mwaka 1996,Burkina Faso ilipewa nafasi ya kuandaa michuano hiyo lakini ilijitoa na nafasi yake kuchukuliwa na Afrika Kusini, michuano ambayo Afrika Kusini ilichukua ubingwa wake wa kwanza baada ya kuichapa Tunissia 2-1 katika mchezo wa fainali.

CAF inatarajia kutoa tamko rasmi juu ya hatma ya Cameroon kuandaa michuano hiyo ya mwakani katika mkutano wake mkuu utakaofanyika 30 Septemba, Sharm EL Sheikh nchini Misri.