
Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli
Bumbuli amesema kuwa Yanga wao ni watulivu tofauti na watani wao Simba ambao wanajigamba wakati wote wakiongozwa na Haji Manara na kwamba wanafanya vitu vyao wakiangali dakika 90 za mchezo huo mkubwa zaidi kwa ngazi ya klabu nchini Tanzania.
"Sisi tupo kimya kabisa, wao ndio wanajimwambafai mara mchezaji wao ana magoli mawili mara matatu lakini sisi tunajua kuwa hiyo kazi ya mchezaji na anatimiza majukumu yake, mwisho wa siku matokeo yatakuwa ndani ya dakika 90", amesema Bumbuli.
Naye Afisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara amesema kuwa wanafahamu kuwa kwenye soka kuna matokeo matatu, kufungwa, sare na kushinda lakini kwa upande wao kuna matokeo ya aina moja tu ambayo ni ya ushindi.
Kuhusiana na picha zinazosambaa mitandaoni zikionesha muundo wa basi mpya la klabu hiyo, Manara amesema, "Simba ni kubwa kuliko klabu yoyote Tanzania kwa sasa, hivyo haifanyi vitu kwa pupa, basi litakapokamilika litaonekana na litajulikana, kwanza jiulize kwanini lisisambae basi la Yanga?, hapo ndo ujue kuwa Simba ni timu kubwa".
Mchezo wa watani wa jadi (Simba Vs Yanga) utapigwa Jumamosi hii, Januari 4 katika uwanja wa taifa Jijini Dar es Salaam.