
Bondia Anthony Joshua [kulia] akimrushia konde bondia Dominic Breazeale.
Bondia Anthony Joshua raia wa Uingereza amefanikiwa kutetea mkanda wake wa IBF uzito wa juu jana usiku katika mpambano uliofanyika ukumbi wa 02 Arena.
Joshua alimtwanga kwa knock out ya raundi ya saba mpinzani wake raia wa Marekani Dominic Breazeale ambaye hajawahi kupigwa katika mapambano yake yote aliyocheza zaidi ya kutoka sare.
Baada ya ushindi huo wa Joshua dhidi ya Mmarekani huyo aliyekuwa hapigiki mratibu [Promota] wa ngumi za kulipwa duniani Eddie Hearn akasema anataraji sasa Joshua atavaana na bondia mbishi mwenye kipaji na uwezo wa hali ya juu Joseph Parker mwezi wa kumi na moja [Novemba] mwaka huu.
Kabla ya hapo Promota Hearn amemtaka bondia Joshua achukue muda wake kupumzika na kufanya maandalizi ya kutosha kwa kuwa atakutana na mpinzania wake mwezi Novemba kutetea mkanda huo wa IBF uzito wa juu dhidi ya mbabe Joseph Parker ambaye anarekodi ya kucheza mapambano 19 na kushinda yote.
Bondia Joshua kabla ya kupata mapumziko kazi yake nyingine itakuwa ni kwenda kuwa mmoja wa watangazaji na wachambuzi wakati wa michezo itakayoihusisha timu ya ngumi ya GB katika michuano ya Olimpiki ya Rio.
