Akizungumza na East Afriuca Radio, Katibu mkuu wa BFT, Makore Mashaga amesema mpaka sasa wana vijana 45 ambao wanatarajia kuingia kambini kwa ajili ya kuendelea na mazoezi, lakini baada ya muda kutakuwa na mashindano ambayo yatasaidia kupangua kikosi hicho na kupata vijana 15 ambao watakuwa kamili kwa ajili ya kuunda kikosi cha timu ya Taifa kitakachokaa katika kambi ya muda mrefu.
Mashaga amesema, timu hiyo itaweza kushiriki mashindano mbalimbali yaliyo katika kalenda ya Chama cha Ngumi cha Dunia kwa kushirikiana na Chama cha Ngumi cha Afrika pamoja na BFT ili kuweza kukuza mchezo huu hapa nchini.
Mashaga amesema wachezaji hao watakuwa na uzito tofauti ili kuweza kupata wachezaji watakaoshiriki katika uzito ambao unaendana nao ili kuweza kuiwakilisha vizuri nchi.
Mashaga amesema kwa kushirikiana na kamati ya Olimpiki nchini TOC, pamoja na Serikali wamehakikisha wanachagua wachezaji wenye uwezo, nidhamu, moyo wenye uzalendo na afya njema vijana hao waweze kushiriki mashindano hayo wakiwa na maandalizi mazuri.