Alhamisi , 12th Sep , 2019

Nyota wa mbio za magari duniani kwa mara 7, Michael Schumacher, amezinduka baada ya kupoteza fahamu kwa miaka 6.

Michael Schumacher

Hiyo imeelezwa na Nesi ambaye anamhudumia huko Paris Ufaransa ambako alipelekwa kwa mara nyingine tena kwaajili ya matibabu zaidi.

Michael alipata ajali ya kujigonga kichwa kwenye mwamba mwaka 2013 wakati akifanya mchezo wa kuteleza katika barafu katika safu za Milima ya Alps huko Ufaransa na tokea hapo amekuwa akihamishiwa katika Hospitali mbalimbali akipatiwa matibabu.

Maendeleo ya afya kwa nyota huyo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakifanywa kwa siri kubwa na mara ya mwisho taarifa kuhusu Afya yake ilitolewa mwezi Januari mwaka huu na Mke wake siku kadhaa baada ya sherehe ya kuzaliwa kwa Michael.

Katika taarifa hiyo mke wake aliweka wazi juu ya kinachoendelea kwa uchache lakini aliomba faragha zaidi hususani katika maendeleo ya afya na kuvitaka vyombo vya habari kuwa na utulivu wakati sahihi utafika.

Mapema mwezi huu Michael alipelekwa Ufaransa kwaajili ya kubadilishwa seli zilizoharibika ndani ya mwili katika hospitali ya Georges Pompidou, Jijini Paris na taarifa rasmi ni kuwa ameanza kupata ufahamu.

"Ndiyo ninamhudumia, nina wahakikishia kwa sasa ameweza kupata ufahamu,” alisema Nesi huyo ambae hakutaka jina lake kuwekwa wazi.

Vyanzo: Express, The Times