Jumatano , 18th Sep , 2024

Kocha Mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi amesema kikosi chake kipo imara na wanaenda kutafuta alama tatu ugenini dhidi ya KMC FC, kesho.

Azam FC watakuwa ugenini dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo kwenye michezo miwili yote amelazimishwa suluhu dhidi ya JKT Tanzania na Pamba FC.

Akizungumza na waandishi wa habari  Kocha Taoussi amesema wachezaji wake wapo tayari kwa mchezo huo kusaka pointi tatu muhimu ugenini.

Amesema anafurahi zaidi kurejea kwa wachezaji watano waliokuwepo kwenye majukumu ya Taifa, akiwemo Kipa wao Mustafa Mohammed.

“Itakuwa mchezo mzuri na wachezaji wapo tayari kwa ajili ya kutafuta matokeo ya kuondoka na alama tatu kutoka kwa wenyeji wetu KMC,” amesema Taoussi.

Naye Mwakilishi wa wachezaji wa Azam FC, Nathan Chilambo amesema wamejiandaa vizuri kwa mchezo huo huku akisisitiza kuwa makocha wa timu hiyo tayari wamefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo uliopita.

“Kocha amefanya majukumu yake na kazi iliyobakia ni kwetu wachezaji kwenda kukamilisha , Hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu kocha wa KMC anaifahamu vizuri Azam ninaimani tukijituma zaidi tutapata matokeo chanya,” amesema Chilambo.

Amesema matokeo ya michezo miwili iliyopita yamewaumiza kwa sababu malengo yao ni kutwaa ubingwa.