Jumatatu , 29th Jun , 2015

Timu ya Azam Fc imesema itashiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati ngazi ya Klabu maarufu kama Kombe la Kagame bila kuwa na wachezaji wote wa ndani waliokuwa timu ya Taifa.

Akungumza na East Africa Radio, Afisa habari wa Azam FC, Jaffary Iddy Maganga amesema, wachezaji walio timu ya taifa watakuwa katika mapumziko kutokana na kutokuwa na mapumziko mara baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi kuu soka Tanzania Bara.

Maganga amesema, kipindi timu hiyo itakapokuwa katika mashindano ya Kombe la Kagame watakuwa wamepumzika na baada ya hapo watakuwa pamoja kwa ajili ya muendelezo wa mazoezi ya kujiandaa na Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara msimu ujao.

Maganga amesema, timu inaendelea na mazoezi ambayo ni ya mchanganyiko ya timu kubwa na ndogo huku wachezaji wa kigeni wakitarajiwa kurejea wiki hii wakitokeza katika timu zao za taifa kwa ajili ya kuendelea na mazoezi ya kujiandaa na michuano ya Kagame inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai mwaka huu jijini Dar es salaam.