Jumamosi , 25th Jul , 2020

Matumaini ya klabu ya Atalanta ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Italia yamefifia baada ya jana kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya AC Milan waliokua wenyeji wao katika uwanja wa Sanciro.

Kikosi cha Atalanta (Pichani) katika shamra shamra za bao walilofunga katika moja ya mechi ya Serie A.

Atalanta walio katika nafasi ya 2 wakiwa na alama 75 ,wapo nyuma kwa alama 5 dhidi ya vinara Juventus ambao hivi sasa watahitaji alama 2 tu katika michezo mitatu waliobaki nayo ili wafikishe alama 82 ambazo hazitofikiwa na timu yeyote na watautwaa ubingwa wa Serie A kwa mara ya 9 mfululizo.

Ili itwae ubingwa huo Atalanta itawabidi washinde mechi zao mbili zilizosalia ili wafikishe alama 81 huku ikiwaombea Juventus kufungwa michezo yao mitatu iliyobaki kuumaliza msimu.

AC Milan ilitangulia kufunga bao lililofungwa na Hakan Calhanoglu dakika ya 14 kabla ya Duvan Zapata kuisawazishia Atalanta dakika 34, ingawa Ruslan Mislonivsky aliotesha mbawa mkwaju wa penati dakika ya 26 ya mchezo huo.

Kwa upande wa AC Milan chini ya kocha Stefano Pioli imeendeleza mwenendo mzuri wa kutopoteza mechi 11 mfululizo tangu ligi iliporejea mwezi uliopita baada ya janga la Corona ingawa wameshuka hadi nafasi ya 6 katika msimamo wakiwa na alama 60.

Pia kwa upande wa kikosi cha kocha Gian piero Gasperini wa Atalanta wameendeleza rekodi nzuri ya kutopoteza michezo tangu kurejea kwa ligi,kwani ilicheza mechi mechi 11 ,imeshinda mechi 8 na sare michezo 3.

Lakini Atalanta haijapoteza mchezo hata mmoja ya mashindano yote tangu Januari 20 mwaka huu ambapo ilishinda michezo 15 na imetoa sare 4 tu.

Kwa mara ya mwisho kikosi hicho kilipoteza mechi ilikua Januari 20 dhidi ya SPAL ambapo kilikubali kipigo cha bao 2-1.