Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
Akiongea leo kwenye MJADALA wa East Africa Television, Katibu wa Mtandao Wa Wanafunzi Tanzania, Joseph Malekela ameiomba bodi hiyo kuondoa ukomo wa idadi ya wanafunzi kwani sharti hilo linasababisha wanafunzi wengi kukosa elimu ya juu licha ya kuwa na vigezo vyote.
''Hii idadi ni ndogo sana ukilinganisha na wanafunzi waliofaulu kidato cha sita na wanahitaji mkopo, ni sawa na ilivyokuwa mwaka jana ambapo wanafunzi elfu thelathini pekee tu ndio walipata mkopo na kuacha waombaji wengi wakibaki nyumbani'', amesema Malekela.
Malekela amependekeza kuwa kwasababu mkopo huo ni deni na watu wanarudisha inabidi wote wapewe mkopo na sio kuwa na ukomo wa idadi kwa sababu ya sifa zilizowekwa ambazo kuna muda hazina uzito sana kwani kila anayeomba mkopo ana uhitaji.
Hata hivyo Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa Bodi ya mikopo Veneranda Malima, ambaye naye alikuwepo kwenye MJADALA amesema, lazima kuwepo na vigezo ambavyo vinawawezesha kutambua nani apate mkopo na pia lazima viwepo vipaumbele ikiwemo Yatima na wasiojiweza.
Aidha Bi. Veneranda amefafanua kuwa ni ngumu kutoa mkopo kwa wanafunzi wote huku akibainisha kuwa wanafunzi waliokosa mkopo mwaka jana wameomba na wengine wamepata.