Jumanne , 26th Jul , 2022

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mhe. Neema Lugangira siku ya jana Julai 25, 2022 akiwa katika ofisi za East Africa Television na East Africa Radio alizungumza kuhusiana na kampeni ya Namthamini na juhudi zake katika kuwasaidia wanafunzi wa kike nchini waweze kupata taulo za kike za kujistiri

Mhe. Neema Lugangira akiwa studio za East Africa Radio.

Mhe. Lugangira anasema moja ya vitu ambavyo amejikita navyo kwa mwaka huu ni kuona namna gani ambavyo ataweza kupaza sauti serikali iangalie watoto wa kike mashuleni hususani wa mikoani wanaweza vipi kusaidiwa taulo za kike.

''Watoto wanaotoka katika mazingira magumu hususani watoto wa vijijini mara nyingi wanakosa shule siku 5 mpaka 7 kila mwezi kwa sababu tu ya kuwa kwenye hedhi, na wanakosa shule kwa sababu hawana nyenzo sahihi za kujistiri kwa maana ya taulo za kike, na pale ambapo wanakwenda shule wanatumia vitu ambavyo ni hatarishi kwa mfano mabanzi, magazeti, nyasi na vitu ambavyo vinaweza kuwapelekea kuwaweka hatarini kupata kansa'' alisema Mhe. Neema Lugangira.

#

Pia Mhe. Lugangira amesema katika kipindi cha bunge la bajeti 2022/23 lililomalizika hivi karibuni, aliweza kuishauri serikali katika mradi wa maendeleo wa TASAF waone namna ambavyo wataweza kuwasaidia watoto wa kike wanaotoka katika kaya maskini waweze kupata taulo za kike.

Aidha, Mhe. Lugangira ameipongeza East Africa Television na East Africa Radio kwa juhudi zao katika kuwasaidia wanafunzi mashuleni kupitia kampeni ya Namthamini ambayo hufanyika kila mwaka tangu mwaka 2017.

Mhe. Lugangira amepaza sauti mara nyingi bungeni kuhusiana na mtoto wa kike, na mwaka jana kupitia kampeni hii alichangia taulo za kike kwa wanafunzi 42 kwa mwaka mzima.