Mjerumani aeleza alivyompenda Mmaasai

Jumamosi , 6th Mar , 2021

Stephanie Fuchs ni mzaliwa wa nchini Ujerumani, ameeleza safari yake ya mahusiano mpaka ndoa na mume wake Sokoine ambaye ni Mmasai na mkazi wa Kiteto na kusema kuwa walikutana na mume wake huyo miaka 9 iliyopita na alimuona kwenye Kisiwa cha Mafia na kuvutiwa naye.

Stephanie Fuchs akiwa na mume wake Sokoine na mtoto wao

Stephanie ameyaeleza hayo kwenye kipindi cha MadiniDotCom kinachoruka kila siku za Jumamosi kuanzia saa 9:00 hadi saa 10:00 jioni ndani ya East Africa Radio ambapo pia ameeleza jinsi anavyowapenda watanzania kwa kuwa ni wakarimu na wenye upendo.

Stephanie ameeleza pia wakati alivyovutiwa na Sokoine kwa mara ya kwanza kumbe Sokoine naye alikuwa amevutiwa na Stephanie na ndipo baadaye Sokoine alianza kumfuatilia na kisha kumuambia kama anampenda na safari yao ya mahusiano ikaanza rasmi

"Siku ya kwanza kukanyaga kisiwa cha Mafia ndiyo nilikutana na mume wangu Sokoine, yaani hiyo siku nilitembelea tu kijijini kutaka kuona mazingira nikakutana na Masai watatu na nilivyomuona yeye nilimpenda tu, unajua ukimuona mtu sekunde ya kwanza unampenda," ameeleza Stephanie 

Aidha ameongeza kuwa "Nina miaka 11 Tanzania na nina miaka 9 sasa niko na mume wangu Masai, nilikuja hapa Tanzania kufanya volunteering ya utafiti wa mambo ya uhifadhi, nilianza kufanya kazi Ifakara tulikuwa na 'camp' ya wanyama na nilijifunza Kiswahili kule kule".