Ijumaa , 16th Aug , 2019

KABLA ya tarehe 19 Mei, 2019 Nicholaus Jackson Mwandunga hakuwahi kuhudhuria msiba wala mazishi ya ndugu yake yeyote wa damu aliyefariki kwa ajali ya barabarani. Hakuwahi kufiwa na ndugu yake kutokana na ajali ya barabarani, alikua akisikia tu misiba ya aina hii ikiwakumba watu wengine.

Nicholaus (38), hakujua kuwa tarehe hiyo ingebadili kabisa historia yake, kutoka kuwa kaka mwenye wadogo zake watatu mpaka kuwa mtoto mdogo zaidi aliye hai wa Bi. Faith Rahabu Kifwange.

Faraja Mwandunga (35), James Mwandunga (32) na Diana Mwandunga (28) wote walikua wadogo zake, lakini ajali ya gari iliyotokea Jumatano, Alfajiri ya tarehe 19 Mei, 2019 ilikatiza uhai wa wadogo zake wote, akiwemo Diana ambaye alikua mbioni kufunga ndoa siku 7 baadaye.

"Kwa kawaida mwanamke anapoolewa katika familia yetu, huwa tunafanya sherehe mbili za kumuaga (Send off). Moja hufanyika Mbeya alipo mama yetu mzazi na nyingine Dar, ambako ndipo watoto wengi tupo," anaeleza Nicholaus ambaye alinusurika kifo katika ajali iliyochukua uhai wa wadogo zake, huku yeye akizirai na kuzinduka baada ya nusu saa.

Anaeleza kuwa, sherehe ya kumuaga Diana, bibi harusi mtarajiwa ilishafanyika kwa mafanikio nyumbani kwao eneo la Chimala, wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, tarehe 16 Mei 2019 na yeye na ndugu zake walijipanga kurejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya sherehe ya pili  wakitumia usafiri wa gari ndogo aina ya Raum new model, Na. T 251 DGK mali ya kaka yao mkubwa Stephano Mwandunga.

"Bibi harusi mtarajiwa (Diana), hakutakiwa kupanda gari letu, yeye alitakiwa aondoke mapema tarehe 17 Mei kwa ndege na mumewe mtarajiwa lakini alikataa. Akataka kuondoka na sisi, huku mumewe mtarajiwa Elisante Edward akiamua tu kupanda basi la abiria ili kurejea Dar.

"Siku ya tukio tulisafiri kama kilometa 40, tukiwa ndani ya Mbeya, tulipofika Igawa, njia panda ya Mbeya - kuelekea Rujewa, upande wetu tuliokua tunatembea palikua wazi ila mbele yetu katika upande wa gari tunazopishana nazo  tuliona malori mawili yaliyosimama barabarani na huku yakiwa yameachiana umbali wa mita zipatazo 20 kutoka lori moja na lingine. 

Nadhani moja lilikuwa limeharibika na lingine lilisimama kutoa msaada, na kwasababu ya wembamba wa barabara hayakusimama pembeni bali yalikua barabarani," anaeleza Nicholaus na kuendelea;

"Dereva wetu alikua kwenye mwendo mkali wa kilomita kama 90 au 100 hivi tukiteremsha eneo hilo la mlima, lakini ghafla tukaona Fuso likiwa mwendo mkali ilikija katika njia yetu baada ya kuhama upande wake uliokua na malori mawili yaliyosimama bila kuweka alama za tahadhari. Wote tulihamaki."

Gari walilokuwemo lilikua na abiria sita. Watu wazima watano, akiwemo Nicholaus na nduguze wanne, mmoja akiwa ni dereva wao pamoja na mtoto wa miaka miwili, aliyekua mtoto wa mmoja wa wadogo zake.

Nicholaus aliyekua amekaa kitu cha mbele pamoja na dereva anasema, "niliona tukielekea kugongana uso kwa uso na lori. Kwa kua barabara ile ni nyembamba na pembeni ina makorongo ndipo ghafla dereva wetu ili kuepuka kugongana uso kwa uso na Fuso alijaribu kuhama upande wetu ili akajichomeke katika nafasi ndogo iliyokuwepo upande wa pili (kulia) wa barabara yalipokua yamesimama malori mawili na kuacha nafasi kati.

"Kwa kuwa dereva alikua amekata kona kidogo, lile fuso lilikuja kutugonga kwa ubavuni, katika mlango wa abiria wa nyuma ambako ndipo walikuwepo abiria wanne; watu wazima watatu na mtoto.

Tulipogongwa, gari yetu ilisukumwa na kwenda kujibamiza katika malori yaliyokua yamesimama, hivyo mlango mmoja wa viti vya abiria wa nyuma uligongwa na Fuso na mwingine ukaenda kujigonga katika moja ya lori lililokua pembeni."

Nicolaus alizimia palepale kwa dakika takribani 30 kabla ya kuzinduka, na kukuta watu wakiwa wamejaa eneo la tukio na kuwakimbiza hospitali wao, huku wakielezwa kwamba abiria wa nyuma (wadogo zake na mpwa wake), wamekimbizwa hospitali ya rufaa ya Mbeya. Hawakuelezwa kuwa ndugu zao wote wanne wamefariki dunia palepale, mpaka baadaye jioni.

Kwa mujibu  wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kufunga mkanda wa usalama katika gari humsaidia abiria wa mbele kujikinga na madhara ya ajali kwa asilimia 40 mpaka 50 kwa abiria aliye mbele, na asilimia 50-75 kwa abiria waliokaa viti vya nyuma. 

WHO pia wanapendekeza watoto wadogo wawekwe katika vizuizi vya watoto, vinavyowafanya wasitupwe au kuhamishwa kitini iwapo ajali itatokea.

Nilimuuliza Nicholaus kama abiria wote walifunga mikanda wakati wa safari, alisema; yeye na dereva walifunga mikanda, na abiria waliokaa kushoto na kulia katika viti vya nyuma walifunga mikanda lakini bibi harusi aliyekaa katikati ya wenzake katika kiti cha nyuma hakufunga mkanda, wakati mtoto wa miaka miwili alipakatwa tu mikononi na mama yake (Faraja Mwandunga).

"Tuliokua mbele tulipona kwasababu tulifunga mikanda, na gari haikugongwa kwa mbele bali kwa ubavuni kwenye mlango wa viti vya nyuma. Waliokaa mlango wa kushoto na mlango wa kulia nyuma walipata madhara makubwa kwa sababu gari iligongwa mlangoni upande mmoja na upande wa pili wa mlango ukaenda kujibamiza kwenye gari lingine, ila bibi harusi huenda alipoteza maisha kwa kurushwa na kujigonga kwa kua hakufunga mkanda," anaeleza.

Nicholaus amabye pia ni msomi wa Sosholojia, aliyehitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2014, anasema dereva wao Ibrana Mwandunga ni dereva mwenye uzoefu wa miaka miwili ya kuendesha gari ndani ya jiji la Dar, lakini hakuwa na uzoefu wa kuendesha gari katika safari ndefu ikiwemo za mikoani.

Wakati ajali hii ikiondoka na uhai wa watu wanne, wawili walionusurika kifo walibaki majeruhi, Nicholaus akiwa ameumia shingo na kuwekewa kishikiza shingo huku dereva Ibrana akiumia mbavu; hata hivyo wote waliruhusiwa kutoka hospitali na kushiriki mazishi ya ndugu zao tarehe 20 Mei, 2019.

Mpaka sasa Nicholaus bado analalamika maumivu ya shingo, hawezi kugeuza shingo nyuma kwa haraka, na hata kwa taratibu hawezi kugeuka sana. Anasema kifo cha ndugu zake kimewaacha wapweke sana lakini wanamshukuru Mungu kwa wao kunusurika ili walau waeleze kilichotokea.

Anasema maandalizi yote muhimu ya familia ya Mwanduga kumuaga binti yao, ili akaanze maisha ya ndoa na mumewe mtarajiwa Elisante Edward yalikua yamekamilika. Baada ya sherehe ya Send off iliyofanyika Mbeya, tarehe 16 Mei, 2019 na kugaharimu Sh. milioni 7.5, sherehe ya pili, kambambe zaidi ya kumuaga Diana ilikua imepangwa kufanyika Dar es Salaam.

Bajeti yake ikiwa ni Sh. milioni 32, na Kamati ya sherehe ikiwa imeshafanikiwa kukusanya zaidi ya Sh. milioni 18 za michango ya sherehe hiyo iliyopangwa kufanyika Alhamisi ya Juni 26, ambapo ndoa ingekua 29 Juni, 2019. Nilipomuuliza Nicolaus iwapo michango hiyo ya sherehe ilirejeshwa kwa wachangiaji baada ya kifo cha Diana, alisema wachangiaji waliamua michango ya Send off iwe michango ya rambirambi, na itumike kugharamia msiba na mambo mengine.

"Baadhi ya fedha tulishalipa kwa watoa huduma za chakula, ukumbi, MC na muziki ni jambo lililowaduwaza hata wao lakini hapakua na namna. Tuliwazika ndugu zetu na baadaye familia ya Bwana harusi na sisi tulikutana kama ndugu, tukazungumza kuhusu suala hili zito lililotutokea," anasimulia.

Diana, Bi. harusi mtarajiwa anaelezwa kuwa alikua binti mpiganaji kimaisha, na mbunifu. Baada ya kumaliza kusoma Stashahada yake na kutokupata ajira aliamua kuanza biashara akitumia mitandao ya kijamii (Online shopping).

"Alikua akiuza bidhaa mbalimbali mtandaoni ikiwemo michele aliokua akiutoa Mbeya, na akawa anajipatia kipato," anaeleza Nicholaus.

Kwa mujibu wa WHO vijana wa miaka 15 mpaka 29 ndiyo waathirika wakubwa zaidi wa ajali za barabarani, huku ikielezwa kuwa ajali za barabarani zimekua zikisababisha vifo vya watu milioni 1.3 kila mwaka na asilimia 30 ya vifo na ajali hizo hutokea katika nchi za dunia ya tatu.

WHO inakadiria kuwa asilimia tatu ya pato la Taifa nchini Tanzania hutumika kugharamia athari za ajali za barabarani. Hii ni sawa na kusema zaidi ya trilioni nne hupotea kutokana na madhara ya ajali. Taarifa za Jeshi la Polisi nchini zinaonesha kuwa magari binafsi, ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha vifo kutokana na ajali za barabarani kulinganisha na mabasi ya abiria, daladala, malori na pikipiki ambapo kati ya Januari na Juni mwaka 2019 magari binafsi yalipata ajali 528, zilizosababisha vifo 222 na majeruhi 453.

Irene Msellem, mdau wa usalama barabarani anatoa mtazamo wake kuhusu ajali hizi, akisema magari binafsi yenye uzito chini ya tani 3.5 hayajawekewa ukomo wa mwendo kisheria, kwani yanatakiwa kukimbia kilometa 50 kwa saa katika maeneo ya makazi, lakini maeneo yasiyo na makazi wala vibao vya kuelekeza mwendo wanaweza kwenda mwendo wowote ambao dereva ataona unafaa.

"Wadau tunapendekeza kuwa kama ilivyo kwa mabasi na magari mengine makubwa yanavyoadhibiwa kwa kuzidisha kilometa 80 kwa saa, uwekwe pia ukomo katika magari binafsi ambao unaweza kuwa kilometa 100 kwa saa," anasisitiza.