"Hakuna mambo ya tuma na ya kutolea"- Prisca

Alhamisi , 4th Mar , 2021

Mwanamke Kinara Prisca Schulter, amesema kuwa utaratibu uliopo nchini Ujerumani kwa wanandoa ni kwamba mume na mke huwa wanashirikiana katika kuhudumia familia kwa kuhakikisha kila mmoja wao anatoa kiasi cha pesa katika kila mshahara wake kwa ajili ya matumizi ya familia.

Mtanzania anayeishi Ujerumani Prisca Schulter

Prisca ameyasema hayo leo Machi 4, 2021, kwenye kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio, wakati alipohojiwa kuhusu umuhimu kwa mwanamke kufanya kazi yoyote ya halali ili kuweza kuongeza kipato cha familia na kumsaidia mume wake majukumu ya ndani ya nyumba.

"Huku Ujerumani mke na mume mnakadiriana kulingana na mshahara wa kila mmoja wenu yaani kila mmoja ana wajibu wa kuacha pesa kila mwezi, ukipata mshahara kila mtu anatumbukiza kwa ajili ya matumizi ya kila siku ya familia mfano hii ya ada, kodi na mahitaji mengine," amesema Prisca.

Ameongeza kwa kusema kuwa "Yaani mwanamke anatoa pesa na mwanaume anatoa pesa, huku hakuna yale mambo ya tuma na ya kutolea, huku mnaongea mfano mimi nimeolewa na Mjerumani yeye anatoa pesa yake na mimi natoa pesa yangu kila mwezi na inajulikana".